- Ni Michael Collins Wa Marekani, Rubani Wa Apollo 11.

MWANAANGA Michael Collins (90) ambaye ni miongoni mwa wanaanga watatu wa kwanza kusafiri kutoka duniani kwenda kutua mwezi, ameaga dunia nchini kwao Marekani Aprili 28 mwaka huu 2021.

Ukurasa huu ukiwa ni miongoni mwa wadau wa habari za masuala ya anga za juu na sayansi zake, unaangalia jinsi safari hiyo ilivyokuwa, na pia kunukuu maelezo ya mwanaanga huyo katika safari hiyo. 

Ikumbukwe kuwa Collins wakati huo akiwa na umri wa miaka 39, ndiye alikuwa rubani wa chombo cha Apollo 11 katika safari ya kurejea duniani.



JULAI 20, 2019, taaluma ya sayansi ya utafiti wa anga za juu duniani ilisherekea miaka 50 tangu binadamu aliposafiri kutoka duniani kwenda kutua na kutembea kwenye ardhi ya mwezi mwaka 1969.

Safari hiyo na zingine 6 zilizofuatia hiyo kwenda kutua kwenye mwezi, mpaka wakati huu ni zile zilizoandaliwa na shirika la anga za juu la Marekani (NASA).

Aidha, inafurahisha na kutia moyo kwamba zimerejea upya jitihada za mataifa mbalimbali kutaka kutuma watu wao kwenda kuishi kwenye mwezi, kwa ajili ya kuchimba madini ya huko na kuyaleta duniani.

Madini hayo yataweza kutumika katika uundaji bidhaa za viwandani kwa kutumia teknolojia ya kisasa, na hivyo kuzidi kudumisha maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani. 

Katika safari hiyo ya kwanza mwaka 1969, chombo cha anga za juu kilichotumiwa na binadamu katika safari hiyo kilipewa jina la Apollo 11, na ambalo hapa tutaona maana yake.


Apollo ni jina la "Mungu wa Anga" katika tamaduni za Kale wakati wa enzi ya dola za Kigiriki na Kiruma, ambapo pia Mwezi ulikuwa na Mungu wake aliyefahamika kwa jina Diana.

Apollo na Diana walikuwa watoto pacha, na hivyo NASA waliamini kuwa Apollo kutoka duniani alikuwa anakwenda kumsalimia ndugu yake Diana kule kwenye mwezi, na kwamba kule angepokelewa salama salimini.

Aliyeshauri jina hilo la Apollo ni mtaalamu wa masuala ya anga za juu, Dkt. Abe Silverstain, ambaye pia ndiye alisaidia kubuni na kusimamia ujenzi wa mtambo wa kituo kikuu cha kurushia Apollo kwenda anga za juu.

Kituo kikuu hicho cha roketi za anga za juu cha 'Kennedy Space Center,' kipo Jimbo la Florida. 

Dkt. Silverstain mwenye asili ya Uyahudi alizaliwa nchini Marekani, alifariki mwaka 2001 akiwa na umri wa miaka 92.

Katika safari hiyo ya kwanza kwenda kwenye mwezi mwaka 1969, watu 3 waliokwenda huko ni kamanda mkuu wa safari hiyo, Neil Armstrong (mwaka huo akiwa na umri wa miaka 39), msaidizi wake, Edwin Buzz (39), na rubani Michael Collins (39).

Hata hivyo, wakati Armstrong na Buzz walipotelemka na kutembea kwenye ardhi ya mwezi, rubani Collins alisalia ndani ya Apollo akiwasubiri hao wenzake ili wakirejea kwenye chombo hicho safari ya kurejea duniani ianze.

Safari hiyo ya kwenda kwenye mwezi na nyinginezo zilizofuata kwa miaka 3 mfululizo (1970, 1971 na 1972), zilihusisha jumla ya binadamu 21 katika safari 7 za chombo hicho cha Apollo.

Apollo hizo ni namba 11 yenyewe, namba 12, 13, 14, 15, 16, na 17, ambapo namba 13 ilikumbwa na hitilafu kubwa huko anga za juu na kushindwa kutua kwenye mwezi, na hivyo kuvunja safari na kurejea duniani.

Miongoni mwa hao binadamu 21, 6 ambao kimsingi ndio walikuwa marubani wa vyombo hivyo, walikuwa wakisalia ndani ya vyombo hivyo katika anga ya mwezi wakati wenzao 2 wakishuka kutua na kutembea kwenye ardhi ya mwezi.

Pamoja na maelezo mengi ambayo yalishatolewa na yanaendelea kutolewa kuhusiana na safari hizo tangu mwaka huo 1969 hadi mwaka 2019 ambao ulikuwa ni wa 50, nimeona ni vyema tumwangalie rubani Michael Collins ambaye sasa ni marehemu.

Baadhi ya sababu za kumwangalia mwanaanga huyo ni hizi, kwamba:-

1. Alikuwa rubani wa chombo cha anga za juu cha Apollo namba 11, katika safari ya uzinduzi wa safari za binadamu kwenda kutua kwenye mwezi.

2. Alikuwa amepewa amri nzito na wakuu wa NASA iliyomtaka kuondoka na chombo chake kurejea peke yake duniani, endapo wenzake wale wawili wangekumbwa na ajali mbaya pale kwenye mwezi na kushindwa kurejea chomboni.

3. Aliporejea aliandika kitabu maarufu kiitwacho, "Carrying the Fire" (kubeba moto kwenda kwenye mwezi), na ambacho pia tunapata baadhi ya maelezo yake ya kusisimua kuhusiana na safari hiyo ya kwanza ya binadamu kwenda kukanyaga mwezi.

4. Alikuwa amehitimu urubani na kutunukiwa cheti maalumu cha urubani wa kuendesha ndege katika mazingira magumu.

Jina lake lipo kwenye orodha ya kihistoria ya mafanikio hayo ya binadamu katika nyanja ya utafiti wa anga za juu, akiwa amekwisha tunukiwa medani 6, ikiwemo medani ya kutukuka ambayo hutolewa na Rais wa Marekani.

Nishani hiyo ni "Presidential Medan of Freedom," hutolewa kwa mtu al

iyechangia ujasiri wake katika kuhakikisha udumishwaji wa usalama wa taifa, amani, na maendeleo yo
yote ya binadamu kwa maslahi ya umma.

Collins anaeleza hivi:


"Hakika, naweza kusema kuwa siku hiyo ya kuondoka duniani kwenda kwenye mwezi ilikuwa ni kubwa kuliko zote kwenye maisha yangu tangu kuzaliwa.


"Siku hiyo ya Julai 16, 1969 tuliamshwa saa 10 usiku wa kuamkia safari hiyo, ili kujiandaa kwenda ughaibuni.

"Tukiwa watatu, yaani mimi Collins, Armstrong, na Buzz, tulipeana salamu za asubuhi na kuanza harakati kubwa za kujiandaa. 

"Baada ya maandalizi ya kawaida ya kibinadamu, ikiwemo kufanya mazoezi ya viungo, tulikwenda kwenye chumba cha kupima afya zetu ili kuwa tayari.

"Baada ya hapo tulikwenda kupata mlo wa chakula cha kifungua kinywa.

"Baada ya hapo, yaani majira ya saa 12 alfajiri, tuliingia kwenye ukumbi wa mikutano na kukuta wamekusanyika wakuu kibao wa NASA kutoka ngazi zote.

"Akilini mwangu nilijua hiyo ilikuwa siku yangu ya kwenda kufa huko anga za juu; na zaidi sana nilimwangalia Armstrong na kuingiwa na majonzi kwa sababu ya kuhofia usalama wake pale angekuwa wa kwanza kukanyaga ardhi ya mwezi.

"Licha ya NASA kutuhakikishia usalama wetu pale kwenye mwezi, hata hivyo sote watatu tulifahamu kuwa kulikuwa na uwezekano mkubwa binadamu kuzama katika ile ardhi teketeke ya mwezi.

"Tuliketi kwenye eneo letu humo ukumbini, ambamo zilitolewa hotuba mbalimbali za kututia moyo, ikiwemo kuhakikishiwa na wakuu kuwa usalama wetu ulikuwa umezingatia katika utafiti wa kina kuhusu mazingira ya mwezi.

"Niliweza kuangalia kupitia dirishani na kuiona Apollo ikiwa kubwa na ya kutisha, huku ikiunguruma mithili ya kiwanda kikubwa.

"Baada ya kutolewa hotuba kadhaa, tulielekezwa kwenda chumba maalumu ambamo tulivaa mavazi rasmi kwa ajili ya safari za anga za juu.

"Hotuba ya Mkurugenzi Mkuu wa NASA ndiyo ilitupatia ujasiri zaidi, ambao nakumbuka hadi leo hii.

"Katika hotuba hiyo, mkuu alisema kwamba safari ambayo ilisubiriwa na Wamarekani wengi tayari imewadia, na kwamba taifa lote lilikuwa nyuma yetu kushuhudia mtanange ambao tunakwenda kuukabili katika safari hiyo muhimu.

"Alisema NASA ilikuwa imefanya maandalizi yote muhimu, ikiwemo kuhakikisha usalama wetu safarini.

"Mkuu aliendelea kueleza kwa kirefu historia ya mtiririko wa mambo na matukio kwelekea siku hiyo, ikiwemo uundaji wa Apollo, aina ya mavazi tutakayovaa safarini, vyakula, malazi yenu ndani ya chombo hicho, na mengineyo mengi.

"Alitaja sifa za kila mmoja wetu, ambazo zilipelekea kuchaguliwa kuwa wa kwanza kwenda kuukabili mwezi.

"Akihitimisha hotuba yake, mkuu huyo wa NASA alisema:

'Sisi NASA, kwa upande wetu, tumekamilisha majukumu yetu katika safari hii; tunabaki tu duniani kuwafuatilia huko anga za juu.

'Chombo cha Apollo kina nguvu kubwa kupita kiasi, lakini hakikisha mnakidhibiti, na si chenyewe kiwadhibiti ninyi binaadamu.

'Chunga muda na kasi ya chombo ili msijikute mkipishana na mwezi.

'Mpaka hapo naweza kusema sasa kazi inabaki kwenu wote 3. Kila la kheri safarini,' alihitimisha.

"Wageni waalikwa walipiga makofi na kusimama wima kutoka kwenye viti vyao, ambapo taratibu sisi tulisimama na kuanza kuondoka kwelekea mlangoni ili tutoke nje na kwenda kupanda chombo tayari kwa safari.

"Tulipotoka nje tulikuta umati wa watu wakitupungia mikono huku sisi tukijibu, ambapo pia tuliingia kwenye gari ambayo ilitusogeza hadi kwenye mlango wa Apollo.

"Huku tukifuatana na ofisa mmoja wa NASA, tuliingia ndani ya lifti ambayo ilitumia sekunde 40 kutuyanyua hadi mlango wa kuingia ndani kabisa ya Apollo. 

"Kumbuka Apollo ilikuwa na urefu wa mita 110 kwenda juu, hivyo chumba chetu wanaanga kilikuwa jirani kabisa na ncha ya chombo hicho.

"Tuliingia ndani ya chombo hicho, ambapo tuliketi nyema na kusubiri saa ya chombo kuondoka; yaani saa 3 asubuhi ya Julai 16, 1969.

"Ofisa aliyetusindikiza hadi chomboni alituaga kwa kutwambia, 'guys take care,' (jamani kuweni makini).

"Tulisubiri tukiwa kimya, huku tukiangalia-angalia mitambo na vifaa kadhaa, ilimradi muda uzidi kusogea tuanze safari.

"Muongozaji mkuu wa Apollo akiwa kwenye chumba cha duniani kwa ajili ya kutuongoza, alituuliza kila mmoja wetu tunajisikiaje kiafya na kisaikolojia, tukamjibu tupo tayari kabisa.

"Ilipotimu saa 3:32 asubuhi tuliarifiwa kuwa Apollo inaondoka, na ghafla na kwa kasi kubwa tuliondoka duniani kwenda kwenye mwezi.

"Mara moja tulishika hatamu ya kukithibiti chombo hicho kikubwa, tukisoma alama zote kwenye chumba cha mitambo kilichoitwa 'Command Module' (chumba cha kwendesha Apollo).

"Apollo ikiwa na uzito wa kilo milioni 3 pamoja na nishati ya mafuta mengi, iliondoka duniani kwa kasi kubwa ya kilomita 40,000 kwa saa, sawa na kasi ya kilomita 11 kwa sekunde.

"Uzito huo mkubwa ulichangiwa na ukubwa wa roketi za kukiwezesha chombo kuwa na kasi ya kuishida nguvuasili ya uvutano ya dunia, na kiasi kingi cha nishati ya mafuta na hewa za gesi, kwa ajili ya matumizi ya safari.

"Wakati chombo hicho kikipaa kwa kasi, tuliomo ndani tulitulia kimya na kuangalia kompyuta zikielekeza.

"Binafsi nilitarajia tukio baya la mlipuko kutokea na kututeketeza sawia, lakini kumbe nilikuwa na mawazo potofu tu.

"Ndani ya muda mfupi tuliweza kuchana ule ukanda hatari wa tabaka la 'ozone' na kutokea anga ya juu kabisa.

"Majira ya mchana wa saa 8 hivi chombo kilifika katika anga tulivu, ambapo kama ilivyokuwa imepangwa kilikupunguza mwendo na kusimama angani, huku kikielea katika anga hiyo.

"Hapo lilifanyika zoezi gumu na la hatari, kwani kachombo kadogo ambako ndiko kangetumiwa na akina Armstrong na Buzz kushuka hadi kutua mwezini kalikuwa katikati ya Apollo, hivyo ilibidi kukachomoa kutoka hapo ili kukaleta mbele kabisa ya Apollo.

"Zoezi hilo lilifanyika kama ilivyopangwa, ambapo tulifaulu kukaleta kachombo hako upande wa mbele ili tutakapofika kwenye anga ya mwezi iwe rahisi kukaachanisha na chombo kikuu cha safari.

"Mipango ilikuwa kuwa wakati Apollo itakapowasili katika anga ya mwezi, Armstrong na Buzz wangeingia kwenye kachombo hako ili kaweze kuwashusha hadi kutua katika mwezi.

"Mimi ningebaki ndani ya Apollo wakati ikiendelea kuelea kwenye anga ya mwezi nikiwasubiri wanaanga hao wapae wakiwa ndani ya kachombo hako, na kuja kukaunganisha na Apollo ili tuanze safari ya kurejea duniani.

"Baada ya kuunganisha kachombo hako na Apollo tungefaulisha (kutoka kwenye kachombo hako) shehena ya mchanga na mawe walivyokusanya kule mwezini, ili tuvilete duniani kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara duniani.

"Baada ya kufaulisha shehena hiyo, kachombo hako tunge kasukuma kaambae hadi kuanguka kwenye ardhi ya mwezi na kulipuka.

"Zoezi hilo lingewezesha Apollo kuzidi kupungua uzito na kuondoka kwa kasi kutoka anga ya mwezi kurejea duniani, huku pia ikiwa ni nyepesi.

"Hivyo, hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya kukachomoa kachombo hako kutoka katikati ya Apollo na kukatanguliza mbele.

"Pia, wakati tukiwa tumesimama kwa muda kwenye eneo hilo la anga ya dunia majira hayo ya saa 8 mchana kwa saa za duniani, tulikula chakula na kisha kukagua mfumo wote wa Apollo ili kuhakiki uimara wa chombo hicho.

"Chakula kilikuwa kimewekwa kwenye paketi ndogondogo, sawa na paketi za 'take away', huku kila mlo ukiwa imeandikwa siku na muda wa kutumiwa.

"Mfano kwamba, mkate, chai na juisi vitumike asubuhi ya tarehe fulani; chapati, mchuzi na nyama ni chakula cha mchana wa siku na saa fulani; wali, kuku, mchuzi na tunda ni chakula cha siku ya tarehe tajwa na saa husika.

"Hivyo, kwa vile vyakula vyote vilikuwa ni vikavu (vimekaushwa), tulitakiwa kupasha maji ya moto na kuvitumbikiza humo na kisha kula kama mlo laini wa kawaida.

"Aidha, katika kusafisha kinywa, tulitafuna kitu kama big-G maalumu ya kusafisha kinywa na kutema kwenye mifuko maalumu ya plastiki.

"Katika kujisaidia, kulikuwa tishu na kachumba kadogo hivi ambako tulijibanza humo na kujisaidia ndani ya mifuko ya plastiki ikiwa na dawa ya kuua vimelea.

"Kama ni mkojo, kulikuwa na kijisehemu ambamo tulijisaidia, na kisha mkojo huo kupitishwa kwenye bomba na kutolewa nje ambapo ulisambaratishwa katika anga.

Pia, "mabaki ya chakula, choo kubwa, nk, viliwekwa kwenye hiyo mifuko ya plastiki ili turejee navyo duniani kuepuka kuchafua anga.

"Katika kufanyia chumba usafi, tuliweza kuwasha vitufe maalumu ambavyo vilitoa upepo mkali chumbani na kufyonza kila kitu kisichotakiwa chumbani na kuingizwa kwenye mifuko maalumu ya plastiki na kuhifadhiwa chomboni.

"Chumba kilikuwa kikubwa kiasi, ambapo kila mmoja wetu alikuwa na kitanda chake ambamo tuliweza kupumzika wakati chombo kikiendelea na safari kama kawaida.

"Katika kulala tulipeana zamu, ili mmoja abaki macho kuweza kufuatilia hesabu za kompyuta ndani ya chombo hicho.

"Ndani ya chumba hicho kulikuwa na kompyuta 2 zenye kusoma taarifa zinazofanana; hiyo ikiwa na maana kwamba kasoro yoyote; mathalani, kutofautiana kompyuta hizo, mara moja tungeweza kubaini kasoro na kutoa taarifa kwa waongozaji wetu.

"Kadhalika, chumba cha kutuongoza kilikuwa na kompyuta kama hizo, katika kufuatilia safari hiyo kupitia taarifa zinazofaa.

"Kuna wakati tulisafiri bila kuuona mwezi, ingawa muda mwingi tulikuwa tumeulenga moja kwa moja ili tukutane nao huko anga ya juu.

"Ndipo siku ya 3 safarini katika kuamkia siku ya 4 ya kutua mwezini, tulitokewa na kitu cha kustaajabisha nje ya chombo chetu.

"Kitu hicho ni mfano wa chombo cha anga ambacho kilikuwa na mwanga mkali mno, huku kikimudu kwenda sambamba na kasi ya Apollo ambayo wakati huo ilikuwa ni kilomita 26,000 kwa saa.

"Mwendo wa Apollo wakati huo ni ule unaoitwa "transonic speed" (kasi sawa na kasi ya sauti), ambapo licha ya kutouona mwezi wakati huo, pia tulitarajia kuanza kujiandaa kutua.

"Chombo hicho cha kigeni kilikatiza mbele ya Apollo na kuizunguka na kukaa sambamba nayo, kama vile gari moja ikitaka kuovateki nyingine.

"Mara moja tulitoa taarifa duniani kwa chumba cha kuongoza Apollo, huku tukiwa na woga, kwamba kuna chombo cha kigeni kimetutokea na kinakwenda sambamba na Apollo.

"Muongozaji mkuu wa Apollo duniani alihoji maswali kadhaa na kisha kujibu kwamba hiyo ni UFO, na kuongeza kuwa 'achana nacho, nyie zingatia safari tu, mpo jirani na anga ya mwezi.'

"Muongoza Apollo alisema kuwa tuwaachie wao NASA kazi ya kufuatilia chombo hicho cha kigeni.

"Punde tu hivi chombo hicho cha kigeni kilikula kona na kupotea kwenda kusikojulikana.

"Baadaye tulijishangaa kwa nini hatukukumbuka tena kuulizia NASA kuhusiana na chombo kile.

"Tuliingia kulala, lakini asubuhi niliamka na kushangaa kuuona mwezi ukiwa mkubwa kupita kawaida na ukiwa tayari upo chini ya anga badala ya kuwa juu kama ilivyozoeleka.

"Tulielekezwa na waongozaji wetu wa duniani kuwa tayari kwa vile tayari tupo kwenye anga ya mwezi, na kutakiwa kuanza zoezi la kupunguza mwendo wa Apollo ili tuweze kufanya maandalizi ya kutua.

"Hiyo ikiwa ni siku ya 4 tangu tulipoondoka duniani, ndipo Armstrong na Buzz halihamia kwenye kale kachombo kadogo tayari kushuka kwenda kutua kwenye mwezi.

"Niliwatakia kheri kwa kuwaambia 'hey, guys take care!' (kuweni makini), waliitikia kwa kusema 'goodbye!' (kwa heri).

"Punde tu hivi, kwa mujibu wa ratiba tuliyopewa, nilibonyeza kitufe cha kufyatua kale kachombo ili kaachane na Apollo na kushuka kwenda kuikabili ardhi ya mwezi na kutua juu yake.

"Zoezi hilo lilifaulu vyema, huku nikisalia ndani ya Apollo kwendalea kuzunguka-zunguka kwenye anga ya mwezi nikiwasubiri hao marafiki zangu warejee ili tuanze safari ya kurejea duniani.

"Hakika, nilijawa na mawazo mengi, na kukumbuka ule usemi wa wakuu wa NASA kwamba 'kama akina Armstrong watakwama mwezini, wewe utapewa amri ya kuondoka pekee yako kurejea duniani na kuwaacha huko.' 

"Hiyo ingemaanisha kuwa Armstrong na Buzz wameangamia peke yao pale kwenye ardhi ya mwezi. 

"Hata hivyo, baadaye sana nilipokea wito kutoka kwao akina Armstrong wakisema wanarejea kwa Apollo (kutoka kwenye mwezi).

"Nilijawa na furaha pale nilipoona kale kachombo kadogo kalikowabeba kakija kuungana na Apollo.

"Baada ya maandalizi yote kukamilika, ikiwemo kutumia mpira wenye upepo mkali ili kupuliza vumbi la mwezini kutoka kwenye mavazi yao, safari ya kurejea nyumbani ilianza mara moja.

"Nilifyatua kitufe cha kuiondoa Apollo kutoka anga ya mwezi, ambapo punde tu hivi chombo hicho kilishika kasi yake 'kupaa' kutoka kwenye anga ya mwezi kuelekea duniani.

"Nasema tulipaa kutoka kwenye mwezi kuja duniani, kwa vile wakati tukiwa hapo kwenye mwezi tuliiona dunia ikiwa juu kama vile tunavyouona mwezi tukiwa duniani.

"Tofauti ni kuwa dunia ilionekana kubwa na ikiwa na rangi nzuri ya bluu, ambapo ilipita taratibu juu ya anga ya mwezi kama hivi tunavyouona mwezi ukipita kwenye anga ya dunia.

"Hatimaye siku ya 8 tangu tulipoondoka duniani kwenda kwenye mwezi, tuliweza kuwasili duniani na kupokewa kwa shangwe kubwa.

"Tuliingizwa kwenye chumba maalumu kwa uchunguzi wa kiafya, ambapo kwa siku 21 tulikuwa kwenye karantini mahsusi.

"Baada ya kukamilika karantini hiyo tuliachiwa huru na kurejea uraia kuungana na familia zetu, na kwendalea na maisha kama kawaida.

"Tukiwa uraiani tulitoa mihadhara mingi, huku pia wanasayansi wakitumia maelezo yetu katika kuandika vitabu na makala mbalimbali kuhusiana na uhalisia wa jiografia na pia yalivyo mazingira ya mwezi."

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA YA MKWAWA AMBAYE ALIWAHI KUWA CHIFU WA UHEHE HISTORIA YA MKWAWA Mkwawa alikuwa kiomgozi wa jadi wa kabila la wahehe nchini Tanzania, ni moja kati ya viongozi shupavu wa jadi waliowahi kuishi duniani japo mapokeo yao yanaharibiwa taratibu na mabadiliko ya sayansi na technolojia lakini kumbukumbu zao hazitasahauliki hata vizazi vingi vijavyo. miongoni mwa machifu wanaotajwa kuwa na nguvu za kiutawala kwa kipindi hicho ni pamoja na kinjekitile ngwale wa songea aliyeongoza vita za majimaji, Mirambo wa Tabora nk PICHA YA MKWAWA

Nigeria, Rwanda ruksa kutoka nje, ni baada ya Lockdown

Mwili wa George Floyd kuzikwa leo, maelfu wafurika kanisa la ‘The Fountain of Praise’ kutoa heshima za mwisho