Urithi utakaoishi alioacha Mkapa
WAKATI Afrika na dunia ikiendelea kumlilia Rais mstaafu Benjamin Mkapa (81) aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Julai 24, viongozi mbalimbali wameelezea mchango wake kwa taifa wakisema ni urithi utakaoendelea kuishi baada ya yeye kumaliza safari yake duniani.
Mkapa ambaye anatarajiwa kuzikwa kijijini kwake Lupaso Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara Juni 29, mbali na marais mbalimbali na viongozi wengine wa kimataifa ambao wameeleza kumkumbuka Mkapa kwa mchango wake wa kidiplomasia, viongozi wengine nchini pia wameeleza mambo ambayo yatazidi kukumbukwa daima.
Mkapa aliyeshika nyadhifa mbalimbali kabla ya mwaka 1995 alipokuwa Rais, katika uongozi wake anatajwa kama mtu aliyejenga mifumo ya kitaasisi, kuinua sekta binafsi, kuanzisha taasisi kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), kuanzisha uchimbaji mkubwa wa madini, kuinua diplomasia ya kiuchimi na kuboresha mfumo wa elimu uliosaidia watoto wengi kuanza kuandikishwa shuleni na elimu ya juu.
Kwa mujibu wa viongozi mbalimbali waliomuelezea, walisema Mkapa alikuwa mlezi wa wa nchi, msuluhishi, mwana diplomasia, mchapakazi, mvumilivu, asiyetaka kuingilia mambo ya watu, aliyeamini katika weledi, aliyekijenga Chama Cha Mapinduzi na aliyefanya kazi kwa kujitolea, mzalendo mtu wa kujituma na aliyesaidia kufufua Jumuiya ya Afrika Mashariki, aliyesikia ushauri na asiyesita kutoa mamuzi pale palipohitajika.
DK. SHEIN
Dk. Shein ambaye aliwasili nyumbani kwa Mkapa saa 5 asubuhi alisema, atakumbukwa kwa mazuri mengi aliyoifanyia Tanzania.
Alisema ni kiongozi mahiri aliyefanya naye kazi kwa miaka minne na nusu na kujifunza mambo mengi.
Alisema Mkapa aliifikisha Tanzania mahala pazuri kwa kusimamia misingi ya uchumi ambayo hatimaye ilichangia Tanzania kuimarika.
Dk. Shein alisema Mkapa aliitumikia nchi kwa nidhamu kubwa ikiwa ni pamoja na kiuchumi na kimaendeleo kwa misingi ya amani na utulivu.
Alisema kuwa msiba huo ni wa Watanzania wote na kwa kila anayependa maendeleo ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akisisitiza kumwombea ili apumzike salama.
Aliwataka viongozi wengine kujifunza uongozi kutoka kwa Mkapa kwani kiongozi huyo aliishi vizuri na watu wa maeneo yote bila kuwabagua.
Alisema anayakumbuka mengi aliyoyafanya Rais Mkapa wakati anafanya naye kazi ikiwa ni pamoja na kusaidia kuibadilisha nchi kwa kufanya mabadiliko ya kiuchumi sambamba na kuimarisha utawala bora kwa kuanzisha Wizara ya Utawala Bora ambayo ilikuwa ndiyo wizara ya mwanzo katika Serikali za nchi za Bara la Afrika huku akisimamia kwa vitendo uchumi wa Tanzania.
Aidha alisema wakati Rais Mkapa anaingia madarakani makusanyo yalikuwa madogo kwani yalikuwa ni wastani wa Sh bilioni 1.7 mwaka 2005 lakini kutokana na juhudi zake yaliimarika zaidi hatua ambayo ilisaidia kufanyika kwa mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
“Ninayakumbuka mengi sana aliyoyafanya Rais Mkapa tukiwa pamoja Serikalini, na ni muhali kuyasema hapa yote kwa muda huu mfupi kwani amefanya mambo mengi wakati nashirikiana naye,” alisema Dk. Shein.
Dk. Shein alisema kubwa kabisa na la muhimu alilofanya Rais Mkapa ni kusimamia mwenendo mzuri wa uchumi wa nchi kutokana na uzoefu wake wa uongozi.
Alisema alifanya kazi kwa kumuheshimu na kuishi naye vizuri na kumuacha afanye kazi zake bila ya kumuingilia kutokana na kumuamini wakati wote.
“Kwa vile alikuwa ananiamini, mtakumbuka hata mwaka 2003 alipokwenda nje ya nchi kwa muda kidogo, mimi niliweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kutokana na mafunzo yake aliyonipa……..ni mtu ambaye ukifanya naye kazi unaona raha sana”, alisema Dk. Shein.
Alisema hali hiyo ilimfanya afanye kazi kwa kujiamini na kusisitiza kuwa Rais Mkapa ni mtu aliyekuwa akishaurika.
MWINYI
Rais mstaafu, Ally Hassan Mwinyi, alisema Mkapa alikuwa mchapakazi, mvumilivu ambaye hakutaka kuingilia mambo ya watu.
“Ndugu yetu huyu alikuwa mtu mzuri sana, kuondoka kwake kwa ghafla kumezidisha masikitiko yetu, alikuwa mtu mchapakazi, mvumilivu, ni mtu ambaye hakutaka kuingilia mambo ya watu alishughulika na yake ambayo aliyafanya vizuri.
“Tumekuwa naye kwa muda mrefu, tumefanya kazi naye, kama mimi nimefanya kazi naye tokea wakati wa mzee marehemu Mwalimu Nyerere, tunasikitika sana lililobakia ni kuvumilia, mambo haya si mtu mmoja yanatufika sote,” alisema Mwinyi.
MAKAMU WA RAIS
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema Mkapa alikuwa msuluhishi kitaifa na kimataifa na kushauri viongozi kuafuata nyendo zake.
“Ni pigo kubwa kwa nchi yetu na Afrika, alikuwa mlezi wa nchi pale ambapo kuna jambo kubwa la nchi akisimamia tunajua suluhu itapatikana.
“Tumepokea simu nyingi kwa marafiki Afrika, wamepata mshtuko, ni kazi ya Mungu na siye hatuna budi kuipokea, tumepoteza mtu muhimu lakini cha maana sasa ni kufuata nyendo zake, tuahidi kuiendeleza Tanzania kama maono yake yalivyokuwa,” alisema Samia.
JENERALI WAITARA
Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali George Waitara, alisema Mkapa alikuwa kiongozi mahiri, makini na hodari katika uongozi wake.
Alisema Mkapa alikuwa anasikia ushauri na hakusita kutoa mamuzi pale palipohitajika na kwamba kitaifa alikuwa bado anahitajika kwa ushauri.
“Nimemfahamu kwa muda, yeye ndiye aliyeniteua kuwa mkuu wa majeshi ya ulinzi Tanzania mwaka 2001, nakumbuka alipoaniambia ananiteua nilikuwa nimepigwa butwaa kidogo na akagundua kwamba ninasita kukubali.
“Alikuwa anasema ni lazima anieleze kwanza, aliniambia nafasi hii lazima mtu mmoja aishike na nimekuteua wewe, alisema hata urais ni kazi ngumu sana angetamani mtu mwingine aichukue nafasi hiyo lakini hana jinsi.
“Baada ya kuniapisha nilimuomba anisaidie maana jeshi kidogo lilikuwa na matatizo, hakusita, amefanya mambo mengi sana.
“Huduma jeshini zilirudi na kila wakati aliniamini nilipokuwa nikimshauri kuhusu masuala ya jeshi na ulinzi kwa ujumla, alinisaidia katika kulisimamia na kuliongoza jeshi letu,” alisema Jenerali Waitara.
KATIBU MKUU CCM
Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, alisema Mkapa alikijenga chama na kukiacha kikiwa imara.
“Mzee Mkapa yamesemwa mengi kuhusu maisha yake na uongozi na utumishi wake, tunamshukuru Mungu kutujalia kupata kiongozi wa aina yake, vilio vitakoma tu na machozi yatakauka lakini maisha yake, mchango wake na utumishi wake uliotukuka vitakumbukwa milele ingawa si rahisi sana haya tunayosema kuyaenzi kwa vitendo.
“Nawaomba Watanzania tuenzi maisha yake, amejenga chama chetu na kukiacha kikiwa imara, amejenga uchumi wa taifa letu, amesuluhisha migogoro katika bara letu, aliitangaza nchi yetu kwa kufanya kazi ya diplomasia,” alisema Dk. Bashiru.
Alisema wakati Mkapa anaingia madarakani alipata asilimia 60 ya kura lakini mrithi wake Kikwete alipata asilimia 80 na kwamba rekodi hiyo ambayo haijavunjwa inadhihirisha kazi kubwa aliyoifanya kwa miaka 10.
“Kiongozi yeyote ambaye anakiwalisha chama kama rais akitekeleza ilani yake vizuri inakuwa ni msingi wa kukiimarisha chama, alipambana na umaskini, rushwa, na kuimarisha misingi ya uchumi wa kitaifa, alikiacha chama kikiwa na hali nzuri kitaasisi na katika uchaguzi tulishinda vizuri.
“Hili ni pengo la kibinbadamu ambapo wote tunaweza tukaondoka, lakini hajaacha pengo la fikra, msimamo, upendo kwahiyo sisi kazi yetu ni kuenzi yale yaliyo mazuri,” alisema.
KINANA
Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Kinana alisema Mkapa alifanya kazi kubwa kwa kujitolea, uzalendo na kujituma.
“Mimi nimekuwa naye katika nafasi mbalimbali aliyoyapanga yeye na wenzake na timu yake yanafikiwa haraka kuliko mambo ambayo hayana uhusiano wa moja kwa moja na kazi zake.
“Jumuiya ya kimatiafa ilituamini zaidi, alinipa ubunge wa kuteuliwa baada ya kampeni na nilifikiri kwamba haikuwa busara kuchukua nafasi ile, wakapendekeza niwe naibu katibu mkuu wa CCM, aliponiita nikamwambia mheshimiwa rais na mwenyekiti nakuomba sana, kila nilipomuambia aniache alikubali aliridhika,” alisema Kinana.
MAALIM SEIF
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema wataendelea kumkumbuka Mkapa kwa maridhiano yaliyosaidia kuleta muafaka baada ya mauaji yaliyotokea Pemba Januari 26 mwaka 2001.
“Alifanya kazi kuhakikisha muafaka unafikiwa, alikuwa akinialika nyumbani kwake katika hatua za kuleta muafaka Zanzibar. Kwenye kamati zilizokuwa zikishughulikia muafaka alikuwa akizungumza kwa dhati, anaonyesha usoni kwamba anamaanisha kile anachozungumza,” alisema Maalim Seif.
Comments
Post a Comment