Serikali ya Tanzania imetangaza kuwa Marehemu Mzee Benjamin William Mkapa atazikwa kijijini kwake Lupaso, wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Kusini mwa Tanzania.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuanzia siku ya Jumapili, Watanzania wote watapata fursa ya kushiriki shughuli za kuaga zitakazofanyika katika uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam.
Shughuli za kumuaga mzee Mkapa zitafanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia tarehe 26 mpaka tarehe 28, kuanzia Jumapili mpaka Jumanne.
Siku ya Jumapili kuanzia saa nne asubuhi, Kanisa Katoliki litaongoza misa ambayo wakazi wa Dar es Salaam na nje ya mji huo watapata fursa ya kuaga mwili baada ya misa na zoezi hilo litaendelea siku nzima mpaka siku ya Jumatatu siku nzima pia itatumika kwa shughuli hiyo.
Waziri Majaliwa amesema siku ya Jumanne tarehe 28 itakuwa siku ya kuaga kitaifa ambapo viongozi mbalimbali wa serikali nchini , viongozi wa dini, na wananchi.
Baada ya zoezi hilo majira ya alasiri mwili wa Kiongozi mstaafu wa taifa hilo utasafirishwa kwenda wilayani Masasi.
Mwili wa marehemu utatua katika uwanja wa ndege wa Nachingwea na kutoa fursa kwa wakazi wa eneo hilo kuaga mwili wa marehemu.
Waziri Majaliwa amewaambia waandishi wa habari kuwa mwili wa marehemu utapumzishwa Siku ya Jumatano tarehe 29.
Rais mstaafu wa serikali ya awamu ya tatu nchini Tanzania Benjamin William Mkapa amefariki akiwa na miaka 81.
Rais John Pombe Magufuli ametangaza usiku wa kuamkia leo Ijumaa kupitia runinga ya taifa taarifa za kufariki dunia kwa kiongozi huyo wa awamu ya tatu katika hospitali moja jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu.
Rais Magufuli alisema Bw. Mkapa amekuwa akipokea matibabu katika hospitali moja jiji Dar es Salaam, na kuongeza kuwa maelezo zaidi yatatolewa baadae.
''Mzee Benjamin William Mkapa Rais wa awamu ya tatu amefariki. Amefariki kwenye hospitali mjini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa. Niwaombe watanzania tulipokee hili. Taifa limepata msiba mkubwa. Tuendelee kumuombea Mzee wetu Rais Benjamin William Mkapa ambaye ametangulia mbele ya haki," ametangaza rais Magufuli.
mkapa
Taarifa hiyo hata hivyo haikuweka wazi Mzee Mkapa alikuwa akisumbuliwa na maradhi gani.
Katika ukurasa wake rasmi wa mtandao wa Twitter rais Magufuli amemuomboleza Mkapa na kusema atamkumbuka "kwa mapenzi yake makubwa kwa Taifa, ucha Mungu, uchapakazi na utendaji wake katika kujenga uchumi."
Comments
Post a Comment