Waislamu waanza mfungo wa mwezi wa Ramadhan
Waislam waanza mfungo wa mwezi wa Ramadhan
Virusi vya corona kwa kiasi kikubwa vimebadilisha mfumo wa Maisha duniani, huku mataifa yakipambana kwa kila hali kukabiliana na maradhi yanayosababishwa na virusi hivyo vinavyosababisha ugonjwa wa COVID19. Karibu vifo 190,000 vimetokea kutokana na ugonjwa huo, idadi ya walioambukizwa hivi sasa inakaribia milioni 2.7, na pia uchumi wa dunia umeathirika pakubwa.
Waumini wa dini ya Kiislamu kuanzia Kusini Mashariki mwa Asia hadi Mashariki ya Kati na hata Afrika wanaanza mwezi huu mtukufu katikati kadhia ya mapambano haya, kwa kuzuiwa kukusanyika na hata kutoka nje.
Hawaruhusiwi kukusanyika kwa ibada misikitini na hata kufanya mikusanyiko mikubwa ya kifamilia pamoja na marafiki wakati wa futari nyakati za jioni baada ya siku nzima ya mfungo, kama ilivyozoeleka.
Hata hivyo licha ya kitisho kinacholetwa na virusi vya corona, viongozi wa dini na wahafidhina katika mataifa mengi kama Bangladesh, Pakistan na Indonesia ambayo yanakaliwa na idadi kubwa ya Waislamu, wanapuuzilia mbali sheria za kutokukusanyika na kuendelea kwenda misikitini.
Maelfu ya watu walihudhuria ibada ya jioni jana Alhamisi iliyofanyika kwenye msikiti mkubwa uliopo kwenye mji mkuu wa Indonesia na kulishuhudiwa mikusanyiko kama hiyo katika maeneo mengi nchini Pakistan.
Comments
Post a Comment