- Ni Michael Collins Wa Marekani, Rubani Wa Apollo 11. MWANAANGA Michael Collins (90) ambaye ni miongoni mwa wanaanga watatu wa kwanza kusafiri kutoka duniani kwenda kutua mwezi, ameaga dunia nchini kwao Marekani Aprili 28 mwaka huu 2021. Ukurasa huu ukiwa ni miongoni mwa wadau wa habari za masuala ya anga za juu na sayansi zake, unaangalia jinsi safari hiyo ilivyokuwa, na pia kunukuu maelezo ya mwanaanga huyo katika safari hiyo. Ikumbukwe kuwa Collins wakati huo akiwa na umri wa miaka 39, ndiye alikuwa rubani wa chombo cha Apollo 11 katika safari ya kurejea duniani. JULAI 20, 2019, taaluma ya sayansi ya utafiti wa anga za juu duniani ilisherekea miaka 50 tangu binadamu aliposafiri kutoka duniani kwenda kutua na kutembea kwenye ardhi ya mwezi mwaka 1969. Safari hiyo na zingine 6 zilizofuatia hiyo kwenda kutua kwenye mwezi, mpaka wakati huu ni zile zilizoandaliwa na shirika la anga za juu la Marekani (NASA). Aidha, inafurahisha na kutia moyo kwamba zimerejea upya jitihada za mataifa mb...